Kulingna na gazeti la daily Nation, Bwana Odinga kupitia taarifa iliotolewa na mshauri wake Salim Lone, amesema kuwa serikali ya Jubilee sio halali akiongezea kwamba uamuzi huo wa mahakama ya juu ulifanywa kupitia shinikizo.
Taarifa hiyo ilisema kuwa ”Sisi watu wa Nasa tayari, tulikuwa tumeamua kabla ya uamuzi wa mahakama kwamba hatuitambui serikali ya Uhuru Kenyatta”.
Pia amesema kuwa ”Uamuzi huo haujabadilishwa na uamuzi wa mahakama ya juu ambao haukutushangaza. Ni uamuzi uliotolewa chini ya shinikizo kubwa ,hatushutumu mahakama tunaihurumia”.
Ushindi wa rais Uhuru Kenyatta mnamo mwezi Oktoba 26 uliidhinishwa na mahakama hiyo kupitia uamuzi wa pamoja wa majaji sita wa mahakama ya juu.
Kulingana na gazeti hilo bwana Lone amedai kwamba mahakama ilikutana chini ya shinikizo kubwa, baada ya kushindwa kukutana kutokana na wasiwasi mkubwa wa kiusalama kufuatia kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa dereva wa naibu jaji mkuu kabla ya kusikizwa kwa kesi ya uchaguzi wa tarehe 26 Oktoba.