Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga amependekeza serikali ya muda iundwe nchi humo na kutawala kwa muda wa miezi sita kama sehemu ya kutatua mzozo wa kisiasa nchini humo.

Odinga, ambaye alisusia uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi uliopita, amesema katika kipindi hicho kunafaa kufanyika marekebisho ya katiba kuchunguza upya mamlaka ya rais.

Kiongozi huyo ambaye ameanza ziara nchini Marekani alisema yuko tayari kufanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta kuhusu marekebisho ya kikatiba ambayo anasema yanahitajika kupunguza hatari ya kuzuka kwa fujo kutoka kwa makundi ya jamii za wachache ambao wanajiona kwamba wametengwa.

Kenyatta alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo wa marudio uliofanyika tarehe 26 Oktoba akiwa na kura 7.5 milioni ambazo ni sawa na asilimia 98 ya kura zilizopigwa.
Waliojitokeza kushiriki uchaguzi huo ni asilimia 39 ya waliojiandikisha kuwa wapiga kura nchini humo.

Uchaguzi huo ulitokana na hatua ya Mahakama ya Juu, kufuatia kesi iliyowasilishwa na Bw Odinga, kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa tarehe 8 Agosti ambapo Bw Kenyatta alikuwa ametangazwa mshindi akiwa na asilimia 54 ya kura.

Mahakama ya Juu ilisema uchaguzi huo wa mwanzo ulikumbwa na kasoro nyingi lakini pia alisusia uchaguzi wa marudio akisisitiza lazima mageuzi yafanywe katika Tume ya Uchaguzi (IEBC).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *