Rais wa Marekani, Barack Obama ametoa wito kwa viongozi wakuu wa chama cha Republican kutomuunga mkono mgombea wa chama hicho Donald Trump kutokana na matamshi yake.
Akiongea katika mkutano wa kampeni wa kumuunga mkono mgombea wa chama cha Democratic Hillary Clinton, Bw Obama amesema haina maana kukemea matamshi ya kudhalilisha ya Bw Trump kuwahusu wanawake bila kujitenga na mgombea huyo.
Akihutubu Greensboro, North Carolina, Jumanne jioni, Rais Obama alishangaa ni vipi wanasiasa wa Republican bado wanataka Bw Trump awe rais.
Bw Obama alisema matamshi ya Bw Trump kuhusu wanawake hata yanaweza kumfanya akose hata kazi ya dukani.
Obama alikatizwa mara kadha akitoa hotuba na wapinzani wa Bi Clinton lakini alionekana kutoathirika. Badala yake aliwajibu: “Hii ni demokrasia. Hili ni jambo zuri sana.”
Maafisa wengi wakuu wa chama cha Republican, akiwemo spika wa bunge la wawakilishi Paul Ryan ambaye ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi wa chama hicho aliyechaguliwa, wameshutumu matamshi hayo ya Bw Trump ambaye anaonekana akijigamba kuhusu kudhalilishwa kwa wanawake kwenye video.