Aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama amenunua nyumba mpya katika mji wa Washington DC nchini Marekani.

Nyumba hiyo ina vyumba tisa inapatikana katika mtaa wa kifahari wa Kalorama na iliuzwa $8.1m (£6.2m).

Obama ameamua kuendelea kukaa Washington na familia yake hadi binti yake mdogo, Sasha ambaye ana umri wa miaka 15 amalize masomo ya shule sekondari.

Kiongozi huyo na mkewe Michelle wamekuwa wakizuru mataifa mbalimbali duniani tangu walipoondoka White House mwezi Januari.

Msemaji wa Bw Obama, Kevin Lewis, alithibitisha ununuzi huo na kusema: “Ikizingatiwa kwamba Rais na Bi Obama watakuwa Washington kwa angalau miaka mingine miwili unusu, ina umuhimu kwao kununua nyumba badala ya kuendelea kukodi.”

Kuna vizuizi vya saruji kuzuia watu kufikia nyumba hiyo yenye ukubwa wa futi mraba 8,300 (mita mraba 770), ambayo inalindwa saa 24 kila siku na maafisa wa kikosi cha kulinda marais Marekani.

 Walinunua nyumba hiyo kutoka kwa aliyekuwa afisa wa habari wa Bill Clinton Joe Lockhart, aliyeinunua mwaka 2014 kwa $5.3m.

Nyumba hiyo haiko mbali sana na nyumba ya thamani ya $23m inayomilikiwa na mwanzilishi wa Amazon Jeff Bezos, ambaye pia humiliki gazeti la Washington Post.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *