Rais wa Marekani, Barack Obama na kiongozi wa Ufilipino, Rodrigo Duterte wamekutana ana kwa ana siku moja baada ya kiongozi huyo wa Ufilipino kuonekana kumtusi Bw Obama.
Obama alifutilia mbali mkutano uliokuwa umepangwa kati ya wawili hao baada ya Bw Duterte kumuita mwana wa kahaba.
Walikutana kwa njia isiyo rasmi muda mfupi kabla ya dhifa ya jioni ya viongozi wa nchi za Kusini Mashariki mwa Asia nchini Laos.
Msemaji wa serikali ya Ufilipino amesema alikuwa na furaha sana kwamba mkutano huo ulifanyika.
Maafisa wa Marekani wamesema ulikuwa mkutano mfupi kabla ya dhifa iliyoandaliwa viongozi katika eneo la kuketi viongozi.
Obama na Duterte wanadaiwa kuingia kwenye ukumbi wa dhifa nyakati tofauti na hawakuzungumza au kukaribiana wakati wa hafla hiyo iliyodumu saa moja na dakika 20.