Bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17 serikali imetenga jumla ya Sh bilioni 13.9 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 1,157 kwa shule za msingi na Sh bilioni 11.14 kwa shule za sekondari.
Pamoja na hayo, pia serikali imebainisha iko kwenye mchakato wa kulipa madeni ya walimu kadri yanavyohakikishwa ambapo kwa Oktoba mwaka juzi ililipa madeni ya Sh bilioni 20.12. Mwaka huu inatarajia kulipa madeni yote ambayo ni Sh bilioni 26.04 baada ya mchakato wa kuyahakiki kukamilika tangu Oktoba mwaka jana.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge akiwemo Spika wa Bunge, Job Ndugai, wameitaka serikali kupitia upya ramani ya ujenzi wa nyumba za walimu zinazojengwa kwa sasa, kwa kuwa haziendani na mazingira halisi ya kifamilia.
Hayo yamebainishwa mjini Dodoma jana na Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Juliana Shonza (CCM) aliyetaka kufahamu serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya elimu vijijini kama nyumba za walimu na kulipa malimbikizo ya walimu wanaoidai serikali.
Alisema kupitia mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari (MMES II), serikali imekamilisha ujenzi wa nyumba 146 kati hizo 183 kila moja wataishi walimu sita. Ujenzi wa nyumba hizo umegharimu kiasi cha Sh bilioni 5.5 na zitakamilika Aprili, mwaka huu.
“Serikali pia imeendelea kulipa madeni ya walimu kadri inavyoyahakiki. Katika mwezi Oktoba imelipa jumla ya Sh bilioni 2012 kwa walimu 44,700 na Sh bilioni 1.107 zililipwa Februari mwaka jana kwa walimu 3,221,” alisisitiza Jafo. Alisema kwa sasa walimu wanaidai serikali madeni yanayofikia kiasi cha Sh bilioni 26.04 ambayo tayari mchakato wake wa kuyahakiki umekamilika na mwaka huu, yataanza kulipwa kwa walimu waliopo kazini 37, 620 na walimu wastaafu 2,134.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene, alizitaka halmashauri zote nchini kuweka mikakati bora itakayowezesha ujenzi wa haraka wa nyumba za walimu na madarasa.
Hata hivyo, Spika Ndugai alibainisha kuwa katika jimbo lake la Kongwa, wananchi na walimu hawajazifurahia nyumba za walimu zilizokamilika ambazo zinatumiwa na walimu sita kwa nyumba moja kutokana na walimu hao pamoja na familia zao kubanana kwenye nyumba moja.
Source: Habari Leo