Nyumba ya Mama mzazi wa Wema Sepetu iliyopo maeneo ya Sinza Mori jijini Dar es Salaam imepigwa mawe juu ya bati kwa muda wa saa moja na nusu na watu wasiojulikana.
Mama mzazi huyo ambaye jina lake ni Mriam Sepetu amesea kuwa usiku alikosa raha na kupata hofu kubwa na kuhisi kuna watu wabaya ambao walikuwa wanataka kumvamia na kujikuta akikosa usingizi usiku mzima.
Baada ya kupambazuka alitoa taarifa kwa mwanae Wema na viongozi wengine wa Chadema ambapo Meya wa Ubungo, Boniface Jacob alifika ili kuangalia hali ya mama huyo na kuamua kumuwekea ulinzi.
Meya wa Ubungo Boniface Jacob amesema kuwa wameshaangalia mazingira yote wamegudua kitu ambacho hawatakiweka wazi kwa sasa ila wataweka ulinzi mkali.
Jocob amefafanua zaidi kuwa ulinzi huo hautaishia nyumbani kwa mama Wema, bali hata nyumbani kwa Wema ulinzi utaimarishwa, kwa sababu wamegundua wanachama hao wapya wamekuwa wakiwindwa na watu wasiojulikana.
Kwa upande wake Wema amesema kuwa ameshindwa kuelewa hao watu waliofanya kitendo hicho walikuwa wanataka nini kutoka kwao.