Shiriki la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limetaja aina ya wanachama litakaohudumia baada ya Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kusainiwa na Rais John Magufuli hivi karibuni.
Meneja Kiongozi wa NSSF Mkoa wa Temeke, James Oigo, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waajiri kuhusu sheria hiyo mpya na wajibu wao katika kulinda haki za wanachama.
Watu watakaokuwa wanachama wa NSSF, alisema, ni waajiriwa wote wa sekta binafsi, wageni ambao wameajiriwa Tanzania Bara, waajiriwa katika taasisi za kimataifa zinazofanya kazi Tanzania Bara na watu wote waliojiajiri wenyewe na wale wa sekta isiyo rasmi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya mwaka jana, mifuko ya sekta hiyo imeunganishwa na kubaki miwili – NSSF na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Oigo alisema NSSF inawatembelea wanachama wake nchi nzima kuwaelimisha juu ya sheria hiyo, ili kuondoa hofu iliyopo miongoni mwao baada ya mifuko kuunganishwa na kubaki miwili.
Katika ziara hizo, alisema, NSSF itahimiza waajiri kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati ili kuliwezesha shirika kulipa mafao ya wanachama kwa ufanisi, kuzijua changamoto zinazowakumba waajiri.
Aidha, alisema waliokwishaajiriwa wakati sheria hiyo inaanza ambao walikuwa katika mifuko iliyounganishwa watakuwa wanachama wa mfuko wa PSSSF bila kujali wapo setka binafsi au ya umma.
Aidha, watumishi ambao walikuwa wanachama wa NSSF watabakia kuwa wanachama wa NSSF bila kujali sekta wanayotoka, alisema Oigo.