Mke wa rais wa Nigeria, Aisha Buhari amemtetea mumewe kwa kusema kuwa sio mgonjwa kama watu wanavyosema.
Aisha Buhari ametoa kauli hiyo kuptia akaunti yake ya Twitter akisema kuwa Muhammadu Buhari mwenye umri wa miaka 74 anaendelea na majukumu kama kawaida.
Kauli ya mke huyo wa Rais imekuja baada ya kundi moja la watu mashuhuri kumtaka rais Buhari kuchukua likizo ya matibabu kufuatia wasiwasi kuhusu hali yake ya kiafya.
Ikumbukwe kuwa Machi mwaka huu Rais Buhari alirudi nchini Nigeria baada ya likizo ya matibabu iliochukuwa wiki saba nchini Uingereza ambapo haijulikani alitibiwa ugonjwa gani.
Rais huyo hajaonekana hadharani kwa kipindi cha wiki moja sasa, na hatua ya kutohudhuria mkutano wa baraza la mawaziri pamoja na ibada ya kila wiki ya Waislamu inayofanyika siku ya Ijumaa, imesababisha uvumi zaidi kuhusu hali yake ya kiafya, kundi hilo la watu 13 limesema katika taarifa.
Kundi hilo linashirikisha wanaharakati wenye ushawishi mkubwa akiwemo wakili Femi Falana, mchambuzi wa maswala ya kisiasa Jibrin Ibrahim na kiongozi wa shirika la Transparence International tawi la Nigeria Anwal Musa Rafsanjani.
Raia hao 13 wanasema kuwa walilazimika kumshauri rais Buhari kusikiza ushauri wa daktari wake wa kibinafsi kwa kuchukua mapumziko ili kuangazia afya yake bila kuchelewa.
.