Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungia kwa kipindi kisichojulikana staa wa Hip Hop nchini, Emmanuel Elibariki “Nay wa Mitego” kwa kosa la kuimba nyimbo zisizokuwa na maadili.
Baraza hilo limesema kwamba kifungo hiko ni hadi pale watakapojiridhisha kwamba ametekeleza maagizo yote aliyopewa na baraza sambamba na yeye kubadilika katika kubuni kazi zenye maadili.
Taarifa ya katibu mkuu wa BASATA, Godfrey L. Mngereza, imemtaka Ney wa Mitego kulipa faini ya shilingi milioni 1, na kufanya marekebisho ya mashairi ya wimbo wake wa “Pale Kati”.
Vile vile Staa huyo ameagizwa kuwaomba radhi watanzania kwa kutoa kazi ya muziki yenye kuvunja maadili na kudhalilisha watu wa kada mbalimbali hususani wanawake.
Adhabu hizo zimetolewa baada ya BASATA kufanya kikao cha pamoja na Ney wa Mitego hapo jana.