Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amepinga agizo la Umoja wa Mataifa la kuitaka nchi hiyo isitishe ujenzi wa makazi eneo linalozozaniwa la Wapalesrina.
Taarifa kutoka afisi ya waziri mkuu huyo imesema kuwa Israel haitaheshimu matakwa ya azimio hilo la Umoja wa Mataifa.
Pia taarifa hiyo imesema kuwa Israel inasubiri kwa hamu kufanya kazi kwa ushirikiano na Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump kukabiliana na kile ilisema ni madhara ya azimio hilo.
Katika hatua isiyo ya kawaida Marekani ilisusia kupiga kura kwa azimio la Umoja wa Mataifa, hatua ambayo imewezesha Israel kukosolewa rasmi juu ya vitendo vyake nchini.
Azimio hilo linashutumu Israel kwa kuendelea kujenga kimabavu eneo linalotambuliwa kama sehemu ya Wapalestina.
Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 14 katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Azimio hilo linatambua kuwa hatua ya ujenzi ya Waisrael katika eneo hilo la Wapalestina linalokaliwa kimabavu inatishia mpango wa usoni wa kuunda Taifa la Wapalestina katika mapatano yo yote ya siku za usoni juu ya taifa huru la Wapalestina.