Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa mbalimbali, ikiwemo kuhusu watumishi walioghushi au kutumia vyeti vya watu wengine.
Tangazo hilo la Necta limetolewa kupitia mtandao wake wa tovuti ya www.necta.go.tz ikisisitiza kuwa hatua hiyo, itasaidia kuwafichua watumishi ambao wanatumia vyeti visivyo vyao.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, Necta imewataka wananchi wenye malalamiko au taarifa kuhusu watumishi walioghushi au kutumia vyeti visivyo vyao, kuwasiliana na baraza hilo kupitia barua pepe ya esnecta@necta.go.tz au kupiga simu namba 0742484955.
Wananchi wametakiwa kuwasilisha malalamiko yao kwa kuzingatia muda wa kazi kuanzia saa 2:30 asubuhi hadi saa 10:30 jioni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa.
Hatua hiyo ni moja ya kutekeleza agizo la Rais John Magufuli alilolitoa kwa wakuu wa mikoa Machi 15, mwaka jana la kuhakiki watumishi wa Umma na kuwaondoa watumishi hewa ambao wamekuwa mzigo kwa Serikali.