Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limeunda mfumo wa kutunza taarifa za wanafunzi wa Shule za Msingi (PReM), ambao utasaidia katika uandikishaji wa wanafunzi wote na kupewa namba maalumu, ambayo itamtambulisha mwanafunzi katika ngazi mbalimbali za mafunzo na hivyo kuondoa tatizo la wanafunzi hewa.
Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi alisema mfumo huo pia utasaidia katika uhamisho wa mwanafunzi kutoka shule moja hadi nyingine ndani ya mkoa au nje ya mkoa.
Amesema mfumo huo utarahisisha utaratibu unaotumika sasa wa kuhamisha mwanafunzi kutoka shule moja hadi nyingine na kuweza kuondoa tatizo la wanafunzi hewa na pia utasaidia katika uandaaji na utoaji wa takwimu za wanafunzi katika ngazi ya shule, wilaya, mkoa hadi ngazi ya Kitaifa.
Pia amesema mfumo huo utasaidia katika ufuatiliaji wa taarifa za matokeo ya kila mwanafunzi ili kuhakikisha wadau mbalimbali wa elimu wanapata ufahamu wa kutosha kuhusu ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi ya shule.
Amesema baraza limeanza kufanya majaribio ya mfumo huo katika mikoa miwili ya Mwanza na Ruvuma na ifikapo Desemba mfumo huo utaimarishwa ili Januari hadi Mei mwaka 2017, utumiwe na mikoa yote kusajili wanafunzi wa shule za msingi.