Spika wa Bunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amesema wakati umefika kwa wataalamu na viongozi wa serikali kutumia fedha za serikali kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na sio kujinufaisha wao binafsi.
Ndugai amesema zama zimebadilika na Serikali ya Awamu ya Tano haitamvumilia kiongozi yeyote wa serikali akiwamo diwani atakayetega mirija ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuzitumia fedha kwa mambo yake binafsi.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Deogratius Ndejembi, naye amewaagiza madiwani kuwasimamia wenyeviti wa vijiji na watendaji katika kuwasomea wananchi taarifa za mapato na matumizi na kusimamia migogoro ya ardhi na kuimaliza.
Ofisa wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Kuboja alimtaka Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, White Mwanzalila kusimamia wananchi wasijenge kwenye maeneo ya bondeni hususani katika eneo la Kibaigwa ambalo linakuwa kwa kasi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Ngusa Izengo wakati akijibu swali la Diwani wa Viti Maalumu, Asia Halamga kuhusu mpango wa serikali kwa miradi ya kusambaza umeme kupitia mradi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ameahidi kufikisha umeme kwa taasisi za umma kama shule na hospitali.