Ndege ya Kampuni ya Coastal Aviation iliyobeba watalii 10 imeanguka na kujeruhi watalii wawili na rubani ilipokuwa ikitua katika uwanja wa Lobo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, William Mwakilema amesema ajali hiyo imetokea jana Jumatano Oktoba 25,2017 saa tisa alasiri ilipokuwa ikitua.
Amesema taarifa za awali zinasema chanzo cha ajali hiyo ni mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha iliyosababisha uwanja kujaa maji.
Mwakilema amesema wakati rubani akitua ndipo ndege ilianguka na kusababisha watalii hao wawili kujeruhiwa.
Amesema wanashukuru katika tukio hilo ndege haikuungua na kwamba, ilipokuwa ikiserereka iligonga mti na kusimama.
Mhifadhi huyo amesema mbele kulikuwa na mawe, hivyo ingeyagonga na kulipuka ingesababisha madhara makubwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Mohamed Jafari hajapatikana ili kuzungumzia tukio hilo.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu amesema wanaendelea kulifuatilia na kwamba, wanasubiri taarifa kutoka kwa vyombo vya uchunguzi.