Baada ya migogoro ya ardhi kuendelea kutokea mkoani Morogoro na kusababisha maafa miongoni mwa jamii husika, waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amesema ataongeza askari Polisi na vitendea kazi mkoani humo ili kukabiliana na tatizo hilo.
Waziri Nchemba amesema kuwa serikali haitalinda jadi inayoua watu na kwamba nguvu itatumika kuwasaka wauaji na atakayekamatwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mwigulu amesema hayo wakati alipowahutubia wananchi wa mji wa Mikumi, wilaya ya Kilosa na mjini Ifakara, wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.
Waziri amezitaja wilaya za Kilosa, Mvomero na wilaya ya Morogoro (Halmashauri ya wilaya hiyo) vitendo vya migogoro baina ya wafugaji na wakulima vimekithiri.
Nchemba asema vitendo vya mauaji ya wakulima au wafugaji na jamii nyingine vinavyoendelea katika mkoa huo na hasa kwa wilaya ya kilosa, Mvomero na Morogoro si vya kuchekea na hivyo hatasita kuongeza askari wa kutosha na vitendea kazi ili kupambana na wahalifu hao.
Nao wafugaji wa jamii ya Kimasai wa Mikumi, Mpayane Rombo na Nangai Kasege kwa nyakati tofauti walisema hawatakubali wenzao wachache walete vurugu, hivyo wapo tayari kuwafichua ili washughulikiwe na vyombo vya sheria ili kudumisha amani na utulivu.