Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nay wa Mitego amefunguka mazungumzo aliyozungumza na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamduni na Michezo, Harrison Mwakyembe mjini Dodoma wiki iliyopita.
Katika mauzngumzo hayo Nay amesema kuwa waziri Mwakyembe amemtaka kuimba nyimbo zenye maadili.
Aliyofunguka Nay kuhusu mazungumzo hayo
“Nimeshaonana na Waziri Mwakyembe, kufuatia wito wake, ambapo nilifika hadi kwenye ofisi zake na tuliongea mambo mengi ikiwemo yeye kuniulizia kwa makini tungo yangu hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa katika maongezi yetu alionekana akisifia sana kazi zangu.
“Kubwa zaidi aliloniambia yaani ikiwa pamoja na kunielezea dhamira ya Rais Magufuli, kuachia huru wimbo wangu, baada ya kuusikiliza kwa makini na kubaini hauna dosari ya kuufanya ufungiwe na mimi kunitia hatiani kama ilivyokuwa imechukuliwa na Jeshi la Polisi ambao waliniweka hadi rumande.
“Mwakyembe alisema kuwa rais amesikia wimbo wangu na kufurahishwa na mawazo yangu hivyo akaamua kumuagiza aniachie huru na wimbo uendelee kupigwa, ila aliomba kama kuna uwezekano nitunge wimbo mwingine ambao nitazungumzia mambo mengi ya kijamii ikiwa ni pamoja na juhudi za serikali kupambana na dawa za kulevya.
“Zaidi alisema kuwa kama kuna uwezekano itabidi huu wimbo nifanye remix yake ambayo itanifanya niongeze mistari yenye kuzungumzia janga la madawa ya kulevya, wakwepa kodi na hata wale wote ambao wamekuwa wakipinga harakati za kiuchumi ikiwa sambamba na kuhujumu uchumi wetu.
“Waziri Mwakyembe, amenitaka pia niwe makini zaidi katika kazi yangu kwani nyimbo ambazo nimekuwa nikiimba hakika zimekuwa zikigusa moja kwa moja hisia za watu, jambo ambalo wengine wenye mioyo isiyokuwa na uvumilivu ni rahisi kushindwa kunivumilia na kujikuta wakitaka kunizuru moja kwa moja.