Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari amesema kuwa madiwani wa Chadema mkoani Arusha waliohamia CCM wamepewa rushwa na siyo kumuunga mkono Rais Magufuli.

Nassari ametoa kauli hiyo jana mbele ya waandishi wa habari na kudai kuwa ana ushahidi wa kielektroniki unaoonyesha madiwani hao walivyopewa rushwa ili wajiuzulu nafasi zao.

Mbunge huyo amesema kuwa yupo tayari kujiuzuru ubunge wake kama tuhuma hizo zikiwa na za uongo.

Hata hivyo, diwani wa Kata ya Kimandolu, Mchungaji Rayson Ngowi ambaye amepokewa na Rais Magufuli juzi  baada ya kujiuzulu Chadema akizungumzia tuhuma hizo alisema madai hayo hayana ukweli wowote na kama Nassari ana ushahidi ni vyema angeutoa hadharani.

Ngowi aliwashauri Chadema mkoani Arusha watatue matatizo yaliyopo ndani ya chama hicho na wasitafute visingizio kwa kuwa yeye ameamua kujiuzulu kwa kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli na hajapewa rushwa yoyote.

Diwani mwingine aliyejiengua katika chama hicho wa Kata ya Muriet, Credo Kifukwe amesema hakuna chochote alichopewa kama rushwa kwa lengo la kujiuzulu, akimshauri Nassari autoe hadharani ushahidi anaousema na si kushusha tuhuma zisizo na mashiko.

Nassari amesema ushahidi huo ameuhifadhi ndani ya ‘flash disc’ na yuko tayari kumkabidhi Rais Magufuli na vyombo vya uchunguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *