Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amesema ataendelea kuwa mtiifu kwa Rais John Magufuli, Serikali na Chama cha Mapinduzi tofauti na maneno yanayosemwa mitandaoni.

Tangu alipoachwa kwenye mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, Machi 23, kumekuwa na taarifa nyingi feki kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuenguliwa kwake zikidaiwa kutolewa na mbunge huyo wa Mtama ambazo hata hivyo, amekuwa akizikanusha.

Akizungumza jana wakati akikabidhi ofisi kwa waziri mpya wa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe katika ofisi za wizara hiyo Dodoma bila kutaja maneno hayo ya mitandaoni, Nape amesema ataendelea kumuunga mkono Rais katika dhamira yake njema ya kuleta mageuzi nchini.

Alimshukuru Rais kwa kumpa dhamana ya kusimamia wizara hiyo kwa miezi 15 baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya kwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *