Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye ameshauri vyombo vya usalama nchini vitimize majukumu yao pasipo kutumia nguvu.
Nape amevitaka vyombo hivyo kutotumia nguvu ili iwe kama sehemu ambayo mazungumzo yanaweza kuwa na tija ili kuendelea kulinda nchi katika namna nzuri ya kushirikiana.
Nape amesema kuwa vyombo vya dola ni vyombo vya wananchi kwa hiyo wanatakiwa kutumia busara wakati wa ukamataji na siyo kutumia nguvu wakati wa ufanyaji kazi yao hapa nchini kwa wanawatia mashaka wananchi.
Kauli hiyo ya Nape imekuja kufuatia Polisi kufyatua risasi hewani wakati wanataka kumkamkata aliyekuwa Naibu waziri wa Fedha katika Serikali ya awamu ya nne, Adam Kghoma Malima.
Amesema kuwa “Ni vizuri vyombo vya dola vikatimiza wajibu wao na ni vizuri tukalinda nchi yetu katika mazingira ambayo tumekuwa tukihusiana kwa muda mrefu, vyombo hivi vya dola hivi vimekuwa ni vyombo vya wananchi na ndio maana jeshi letu linaitwa jeshi la Wananchi wa Tanzania, si vizuri kutumia nguvu kubwa pale ambapo hapahitajiki kutumia nguvu kubwa”.
Pia ameongeza kwa kusema “Na mimi nimeendelea kushauri nchi yetu bado tumeendelea kufanya mambo yetu kwa mazungumzo kwa kuelewana”.
Mbali na hilo Nape Nnauye anasema mambo haya ya polisi kutumia nguvu sehemu isipohitajika nguvu yanajenga chuki kati ya wananchi na serikali yao.