Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Nandy ameongea na Rais Samia Suluhu Hassani akiwa jukwaani jijini Dodoma wakati wa Tamasha lake ‘Nandy Festival’ lililofanyika mkoani humo.
Kupitia simu hiyo, kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema anashukuru tamasha hilo kufanyika siku ambayo anatimiza siku 100 tangu alipoapishwa Machi 19, 2021.
“Nina majukumu ya kizazi Dar es Salaam lakini ningekuwepo hapo siku ya leo (jana). Nami nawashukuru leo nikitimiza siku ya 100 mko Dodoma mkitumbuiza vijana, waambie ninawapenda sana,” amesema Rais Samia.
Kwa upande wake Nandy amemshukuru Rais Samia kwa kuonyesha upendo na kumueleza kuwa hakutegemea kama angetumia siku ya ke ya 100 katika uongozi kusherehekea nao.
Baada ya Dodoma Nandy Festival ambayo imekuwa ikifanyika toka mwaka 2017 ataelekea mkoani Arusha.
Nandy ni msanii mwingine wa Bongofleva ambaye tamasha lake limekuwa na mwendelezo na mafanikio baada ya Diamond Platnumz mwenye Wasafi Festival.