Dawa ya kwanza duniani ya kutibu ugonjwa wa kifua kikuu kwa watoto inatarajiwa kuzinduliwa leo jijini Nairobi nchini Kenya.

Kwasasa watoto hutumia dawa zinazotumiwa na watu wazima ambazo hugawanywa kusagwa na kutiwa katika maji.

Mkurugenzi wa maswala ya magonjwa ya watoto katika muungano wa utengezaji wa dawa za TB, Daktari Cherise Scott amesema kuwa dawa hiyo mpya inaweza kuleta afueni kwa watoto milioni moja ambao huambukizwa kifua kikuu kila mwaka.

 Kenya ndilo taifa la kwanza kutoa dawa hiyo mpya kwa raia wake huku mataifa zaidi yakitarajiwa kuendelea na utoaji wa dawa hizo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Dawa hiyo ni mchanganyiko wa dawa tatu zinazotumiwa kutibu Tb zikiwa zimechanganywa kikamilifu na kuwekwa ladha ili kuwavutia watoto.

Inaweza kuyayuka kwa urahisi ndani ya maji hivyo basi kuifanya kuwa rahisi kutumia kila siku katika kipindi cha miezi sita.

Ugonjwa wa kifua kikuu unaongoza miongoni mwa magonjwa hatari dunia na huwaua watu 3000 kila siku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *