Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, amesema amesikia malalamiko ya mwanamuziki Diamond lakini hawezi kumjibu kwa sababu zipo taratibu za kufuata kama anaona hajatendewa haki.

Shonza analijibu hilo ikiwa ni siku moja tangu mwanamuziki  ‘Diamond’ amtaje waziri huyo katika malalamiko yake, akidai amekuwa akikurupuka  na kutolea mfano wa kufungia nyimbo na wasanii wakati akihojiwa na kituo cha redio cha Times.

Waziri huyo amesema hayupo tayari kumjibu Diamond  ingawa wasanii wanapaswa kuelewa kuwa hakuna aliye juu ya sheria hata kama msanii mkubwa namna gani.

Amesema kuwa “Aliyewafungia wasanii si Shonza bali ni mamlaka na kama mlivyoona safari hii hadi Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeingilia kati suala hilo, sasa mtu anaporusha tuhuma kumlaumu Shonza atakuwa hanitendei haki. Isitoshe ofisi zetu zipo wazi anayeona ameonewa afuate taratibu katika kudai haki yake na si kulalamikia pembeni,”.

Kuhusu kutoitwa kwa wasanii kabla ya kufungiwa kwa nyimbo zao Shonza amesema hilo waulizwe Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) maana ndio wenye kujua sababu na kwa baadhi ambao aliwaita ameeleza kuwa ni kutokana na kupewa maagizo ya kubadilisha nyimbo zao na kuwahi kukiri makosa lakini wakashindwa kutekeleza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *