Mwanamuziki wa Taarab, Mzee Yusuf amesema kuwa alipojiunga na Bendi ya East Africa Melody Taarab akiwa mpiga kinanda, ndiyo kipindi ambacho alianza kuwa na uhakika wa yeye na familia yake kula wali kwa kuwa alianza kulipwa 1500.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa mahojiano maalumu na kipindi cha DADAZ cha East Africa Television na kuongeza hata kielimu yeye aliishia kidato cha pili.
“East Africa Melody mimi nimeanza kwa kulipwa 1,500, nimeenda pale nikiwa mpiga kinanda lakini nilikuwa nabeba zile speaker za pale, kila siku tukipiga shoo nne napata hela ya kununua mchele kilo tano napeleka nyumbani, uhakika wa kula wali ndiyo nilianza kuupata kipindi hicho,” ameeleza.
“Watu wanasema huyo ana njaa ndiyo maana amerudi kuimba, kiukweli njaa tunayo sote, kama kweli wanasema hakuna njaa na anayefanya kazi ndiyo ana njaa basi sawa wao waswali tu na walale, mimi naswali na nimejiongeza na napiga na muziki wangu, sijasoma mimi nimeishia Form Two nikaacha, hii ndiyo kazi yangu,“ ameongeza.