Katibu mkuu wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Celestine Mwesigwa amesema bado hawajapata taarifa rasmi ya ukodishwaji wa Yanga kwa Mwenyekiti wake Yusufu Manji.
Mwesigwa amesema TFF inasubili barua rasmi ya ukodishwaji wa Yanga ndipo itoe tamko juu ya ukodishwaji huyo.
Baraza la Wadhamini wa Yanga juzi liliridhia na kumkodisha rasmi timu Mwenyekiti Yusuf Manji kwa miaka kumi kwa ajili ya kuiendesha timu hiyo.
Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Baraka Deusdetit aliithibitishia HabariLeo kuwa baraza hilo la wadhamini chini ya Fatuma Karume limemkabidhi rasmi Manji timu ili ijipange ndani ya miaka 10 timu itakaporejeshwa ijiendeshe yenyewe bila kutegemea wafadhili.
Katika mkutano wa dharura wa klabu hiyo Manji aliomba apewe klabu kwa miaka 10 na katika kipindi hicho atakuwa anachukua asilimia 75 ya mapato ya timu, huku asilimia 25 ikibaki kwa wanachama.
Na katika kipindi hicho cha miaka 10, timu ya soka na nembo ya klabu zote zitakuwa chini yake Manji.
Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la klabu, Francis Kifukwe alisema baada ya wanachama kuridhia mpango huo, wao wanampa pia ridhaa hiyo Manji.