Serikali imesema kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2016, zimezindua jumla ya miradi 1,387 yenye thamani ya shilingi bilion 494.8 na mingine imeanza kutoa huduma kwa wananchi wa Tanzania katika kufanikisha nchi ya uchumi wa kati kupitia miradi hiyo.
Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama, wakati wa kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kilichofanyika wilayani Bariadi mkoani Simiyu.
Amesema miradi hiyo ni ongezeko la asilimia 7.6 kutoka miradi iliyozinduliwa na mbio hizo mwaka jana 2015, ambapo jumla ya miradi 1,343 yenye thamani ya shilingi bilioni 463.5.
Waziri Mhagama amesema kuwa miradi mingi iliyozinduliwa imewahusisha moja kwa moja viojana kwa kuwa ndio nguvu kazi ya taifa ambayo inatarajiwa kutumika kwa ajili ya kufikia uchumi wa katika mpaka ifikapo mwaka 2025.
Aidha Waziri huyo ameongeza kuwa serikali ya awamu ya tano imesema serikali itazisimamia ipasavyo fedha zinazotolewa kwa ajili ya vijana kujikwamua kiuchumi katika halmashauri ili ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwachuhukulia hatua wale wote watakaobainika kufanya ubadhirifu huo.
Pia ameitaja mikoa sita iliyofanya vizuri katika utekelezaji wa malengo ya mbio za mwenge ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya fedha za umma kuwa ni Simiyu, Njombe, Mwanza, Ruvuma, Mbeya na Mtwara.