Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka wadau wa michezo nchini kuwekeza katika sekta ya michezo kwa vijana wadogo wa shule za Sekondari ili kuliletea manufaa makubwa Taifa.
Dkt. Mwakyembe amesema hayo wakati akifungua michezo ya Copa Umisseta ambayo inashirikisha shule za Sekondari za Serikali na Binafsi leo katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
Waziri huyo mwenye dhamana ya michezo amesema kuwa Serikali itahakikisha inawekeza katika michezo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa kuwa michezo ni ajira inayowapatia vijana riziki pamoja na kuchangia katika uchumi wa nchi.
Mwakyembe amesema kuwa amefurahishwa na juhudi zinazofanywa na Kampuni mbalimbali zinazojishughulisha na michezo katika kuhakikisha wanaimarisha sekta ya michezo kwa vijana wadogo wa sekondari.
Mwkyembe amesema kuwa vijana ndiyo taifa la kesho kwa hiyo wanapowekeza kwao lazima watafanikisha kuinua sekta ya michezo nchini.