Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe amesema kuwa amesikitishwa na matamshi ya msanii wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz dhidi ya Naibu Waziri Juliana Shonza.
Mwakyembe amesema kuwa maamuzi ya kuzifungia baadhi ya nyimbo na wasanii wawili kwa kukiuka maadili, yalifanywa kwa mujibu wa sheria na si kwa utashi binafsi wa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo, Juliana Shonza anayemlaumu.
Waziri huyo ameendelea kwa kusema kuwa Diamond atambue kuwa Serikali ina taratibu zake. Maamuzi ya Naibu Waziri ni maamuzi ya Wizara.
Ameendelea kusema kuwa kama ni vikao na wasanii, tumefanya vingi sana, lakini Diamond hahudhurii vikao hivyo na si wajibu wa Serikali kumfanyia kikao chake mwenyewe.
Pia amesema kuwa Hatuwezi kuwa na sheria kwa wasanii wengine na sheria maalum kwake, nadhani hizi ni dalili za kuanza kulewa umaarufu kwani Diamond si Kiongozi wa Shirikisho la Muziki wala msemaji wa Chama cha Muziki wa kizazi kipya kuwasemea wenzake.
Amemalizia kwa kusema kuwa si busara kwake kushindana na Serikali, na kama ana ushauri basi autoe kistaarabu utazingatiwa lakini si kwa kumshambulia Naibu Waziri kwa dharau na kejeli jinsi alivyofanya.