Muuzaji wa madawa ya kulevya maarufu nchini Mexico, Joaquin “El Chapo” Guzman amehamishwa na kukabidhiwa kwa maafisa wa serikali nchini Marekani.
Guzman ambaye huenda akafungwa jela maisha nchini Marekani amekuwa akisakwa na maafisa wa Marekani kwa tuhuma za ulanguzi wa dawa za kulevya ambapo anaingiza kiasi kikubwa cha dawa za kulevya nchini Marekani.
Kiongozi huyo wa genge la Sinaloa alikuwa anakabiliwa na maombi mawili ya kutaka apelekwe Marekani kujibu mashtaka – moja kutoka California na jingine Texas.
Mwaka uliopita alihamishiwa gereza la Ciudad Juarez, ambalo linapatikana maeneo ya mpakani karibu na mji wa El Paso katika jimbo la Texas.
Hata hivyo maafisa walikanusha tuhuma kwamba hatua hiyo ilikuwa kama maandilizi ya kumhamishia Marekani.
Amekuwa akilindwa vikali gerezani ikizingatiwa kwamba alikuwa ametoroka magereza mawili ya ulinzi mkali awali.
Guzman leo anatarajiwa kufikishwa katika mahakama ya dola mjini Brooklyn nchini Marekani kwa makosa hayo ya kufanya biashara haramu.