Muigiza mkongwe wa Marekani, Charmian Carr, aliyeigiza binti mkubwa wa familia ya von Trapp Liesl katika filamu ya The Sound of Music iliyozinduliwa mwaka 1965 amefariki dunia akiwa na miaka 73.
Carr amefariki akiwa mjini Los Angeles baada ya kupata matatizo kutokana na ugonjwa wa dementia.
Baada ya kuondoka kwenye ulingo wa filamu, alianzisha biashara ya kupamba nyumba katika jimbo la California nchini Marekani mpaka umauti unamkuta.
Filamu ya The Sound of Music iliyondaliwa na Rodgers na Hammerstein ilivuma sana, na iliipiku filamu ya Gone with the Wind wakati huo na kuwa filamu iliyozoa kitita kikubwa zaidi cha pesa katika historia kufikia wakati huo.
Carr baadaye aliandika vitabu viwili kuhusu aliyopitia, Forever Liesl (Daima Liesl) na Letters to Liesl (Barua kwa Liesl), na alitokea mara kwa mara katika hafla za kuadhimisha filamu hiyo.
Kushiriki kwake pakubwa katika uigizaji ilikuwa ni katika filamu ya televisheni ya Stephen Sondheim kwa jina Evening Primrose.
Wengi wa mashabiki wa The Sound of Music wamekuwa wakituma salamu za rambirambi kwenye mtandao wa Twitter na pia wameweka sehemu alizoigiza Carr kwenye filamu ya The Sound of Music kwenye mtandao huo.