Mtoto wa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muamar Gaddafi aitwae Saif al-Islam Gaddafi ameachiawa huru baada ya kuzuiliwa kwa miaka sita.
Kuna wasiwasi huenda hatua hiyo ikatikisa zaidi hali ya kisiasa na kiusalama nchini Libya kutokana na kuachiwa kwake.
Saif al-Islam ndiye aliyependelewa na babake kuwa mrithi wake na amekuwa akizuiliwa na kundi la wanamgambo katika mji wa Zintan kwa miaka sita.
Wanamgambo hao wa Abu Bakr al-Siddiq Battalion wamesema aliachiliwa huru Ijumaa lakini bado hajaoneshwa hadharani.
Taarifa nchini Libya zinasema kwa sasa amo katika mji wa Bayda, mashariki mwa Libya, kwa jamaa zake.
Wanamgambo hao wanadaiwa kumuachilia huru baada ya ombi kutoka kwa serikali ya muda ya nchi hiyo.
Serikali hiyo – yenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo – ilikuwa tayari imetoa msamaha kwa Saif al-Islam.
Hata hivyo, alikuwa amehukumiwa kifo na mahakama mjini Tripoli, magharibi mwa nchi hiyo bila yeye kuwepo mahakamani.
Maeneo ya magharibi yanatawaliwa na serikali inayopingana na serikali ya mashariki mwa Libya, lakini serikali hiyo ya magharibi yenye makao yake makuu Tripoli ndiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.