Baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kutoa onyo kwa Mbunge Nassari kuhusu ushahidi anaoutoa kuhusu wateule wa Rais kuwanunua madiwani Arusha, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi, (CUF) Julius Mtatiro ameitaka taasisi hiyo kuchukua hatua na siyo kumtishia mbunge huyo.
Mtatiro ametumia ukurasa wake wa Facebook, kwa kusema kwamba alitegemea TAKUKURU ingempongeza sana Nassari kwa kazi aliyofanya lakini kinyume chake wanamtisha na kumshtaki kwa kauli yake aliyoitoa jana kuwa ataendelea kutoa series ya matukio hayo yanayohusisha rushwa.
Mtatiro ameendelea kusema kwamba TAKUKURU ni chombo cha wananchi, siyo watawala na Nassari ni kiongozi na ni mwananchi, ana haki zote za kuikosoa na kuishinikiza taasisi ya kiuchunguzi ichukue hatua stahiki.
Matatiro ameanza kwa kuandika “TAKUKURU siyo mahakama na kwa kweli haina kinga dhidi ya “kulaumiwa na kushinikizwa na umma”. TAKUKURU ijibu mashinikizo haya kwa kuchukua hatua, aidha kuwafikisha mahakamani wale watoa rushwa au kuwasafisha. Na iache kumtisha Nassari”.
Pia ameendelea kwa kuandika “Kwani Nassari akiendelea kutoa hizo video za ziada anafanya kosa gani kisheria. Kama ni kosa kwa nini wale watuhumiwa (watoa rushwa na wapokeaji) hawajampeleka mahakamani”?
Pamoja na hayo Mtatiro amesema kutokana na kauli za Mkurugenzi wa TAKUKURU haitabaki salama kwa kauli na mienendo ya namna hiyo ikiendelea kutolewa.