Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kwa kushirikiana na Maofisa wa Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini wamefanikiwa kuteketeza mashamba ya bangi ya ukubwa wa zaidi ya ekari 25 na kuwatia mbaroni watu watano.
Watu hao miongoni mwao ni Mwenyekiti wa Kitongoji hicho baada ya kukutwa wakijihusisha na kilimo bangi kwa njia ya umwagiliaji kando kando ya mto Mgeta, katika kijiji cha Masalawe, Kata ya Luale , wilayani Mvomero.
Operesheni hiyo maalumu ya kupambana na dawa za kulevya hasa kilimo cha bangi iliyofanyika Augosti 19, mwaka huu na kuongozwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa , Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe akiwa na Maofisa wa mamlaka ya kuthibiti na kupambana na dawa za kulevya pamoja na viongozi wa wilaya ya Mvomero.
Timu ya Opereshani hiyo ililazimika kuacha magari eneo la kijiji cha Homboza , Kata Mlali na kutembea kwa miguu kwa muda wa zaidi ya saa mbili kufika katika vitongoji vya Lufuna na Tagata vilivyopo kijiji cha Masalawe , kata ya Luale , Tarafa ya Mgeta , wilayani Mvomero kwa ajili ya kutekeleza mashamba hayo.
Kugundulika kwa mashamba hayo ni kufuatia Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya mkoa kupata taarifa kutoka kwa wasiri juu ya uwepo wa uzalishaji mkubwa wa bangi eneo hilo.
Akizubngumza katika eneo la mashamba hayo , Kamishina wa Operesheni wa Mamlaka hiyo, Mihayo Msikhela alisema , opereshani za kutekeleza dawa za kulevya hasa mashamba ya bangi ni endelevu kwenye maeneo mbalimbali nchini na kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama vya mikoa husika.