Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa mara ya kwanza imefanya upasuaji mkubwa kwa mafanikio wa kunyoosha mfupa wa mgongo wa mtoto wa miaka 13 uliokuwa umepinda (kibiongo).
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk Othman Kiloloma amesema jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akielezea upasuaji huo uliofanyika kwa saa tano.
Dk Kiloloma amewaeleza waandishi wa habari kuwa, upasuaji huo umefanyika kwa kutumia teknolojia ijulikanayo kama ‘posterior instrumentation and fusion’ ambayo inahusisha uwekaji wa vyuma maalumu kwenye mfupa wa mgongo katika sehemu ya juu na chini ya mfupa wa mgongo na kuufanya unyooke kama inavyotakiwa.
Amesema uanzishwaji wa upasuaji huo umetokana na kuanzisha kwa ushirikiano wa kimafunzo kati ya Taasisi ya MOI na Chuo cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji cha Afrika Mashariki, Kati na Kusini (COSECSA) na madaktari bingwa kutoka Marekani.
Mkurugenzi huyo amesema uanzishwaji wa upasuaji huo wa kunyoosha migongo ya watoto iliyopinda, unatarajiwa kuisaidia serikali kupunguza rufaa za kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi ambazo ni za gharama kubwa.