Waziri mkuu wa zamani wa Somalia, Mohamed Abdullahi Farmajo amechaguliwa kuwa rais mpya wa Somalia baada ya kumshinda aliyekuwa rais wa nchi hiyo Hassan Sheikh Mohamed kwenye uchaguzi uliofanyika jana.
Farmajo amepata kura 184, Hassan Sheikh akapata kura 97 naye rais mwingine wa zamani Sharif Sheikh Ahmed akapata kura 46.
Mshindi alitakiwa kupata theluthi mbili ya kura zote zilizopigwa lakini kabla ya duru ya tatu kufanyika, Bw Hassan Sheikh alikubali kushindwa na kumpongeza Farmajo.
Baada ya habari za ushindi wake kuanza kuenea, milio ya risasi ilisikika pande mbalimbali za Mogadishu watu wakisherehekea ushindi wake.
Mwanamke wa kwanza kutangaza kuwa angewania urais nchini Somalia ingawa alijiondoa baadaye, Fadumo Dayib ameonekana kufurahia ushindi wa Farmajo.
Taifa la Somalia linalokabiliwa na vita vya kikabila pamoja na vile vya ukoo halijafanikiwa kufanya uchaguzi wa kidemokrasia unaoshirikisha raia kushiriki katika uchaguzi tangu 1969.
Uchaguzi huo ulifuatiliwa na mapinduzi, uongozi wa kiimla na vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoshirikisha koo na wapiganaji wa al-Shabab.