Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL Group), Mohammed Dewji ametaja mambo mawili ambayo anayajutia kwa kutoyafanya na anahisi kuwa amechelewa kuyafanyia maamuzi.

Dewji amesema kuwa kushindwa kuwekeza katika benki na mawasiliano ya simu ni mambo ambayo yanamuumiza kichwa akiendelea kuyajutia.

Mfanyabiashara huyo ametuma sehemu ya mahojiano kwenye mtandao wake wa Twitter akielezea mambo hayo.

Akijibu swali lililotaka atoe ushauri wake nini ambacho hajakifanya Dewji alianza kwa kusema, “Nimekosa mambo mengi katika maeneo ambayo nilipaswa kuwekeza…nilipaswa nimewekeza katika benki. Ingawa sasa najaribu kununua benki lakini nadhani nimechelewa. Na jambo la pili ambako nimekosea ni kwa kushindwa kuwekeza katika biashara ya mawasiliano ya simu.”

Amesema hakuwa na mwamko wa kujiingiza katika uwekezaji wa mtandao wa mawasiliano ya simu kwa vile alihisi wananchi wengi walikuwa hawana uwezo kumudu kununua simu na kuwasiliana.

“Unajua nilikuwa nikifikiri kuwa hivi watu hawa watapata wapi fedha kununua simu lakini sasa ukiangalia kama Tanzania kila mtu anamiliki simu ya mkononi…Haya ndiyo mambo mawili ambayo nayajutia,” amesema mfanyabiashara huyo.

Miongoni mwa wafanyabiashara waliopata mafanikio makubwa kutokana na kuwekeza katika mtandao wa mawasiliano ya simu ni Mo Ibrahim raia wa Uingereza ambaye jarida la Forbes limemtaja kuwa ni mtu 692 kwa watu matajiri duniani.

Mfanyabiashara huyo mwenye asili ya Sudan sasa anasimamia taasisi yake ijulikanayo Mo Ibrahim Foundation ambayo inahimiza dhana ya utawala bora barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *