Mfanyabiashara nchini, Mohammed Dewji (MO) ametajwa kwenye orodha ya mabilionea 21 wa Afrika huku akiwa Mtanzania pekee kwenye orodha hiyo iliyotolewa na Jarida la Forbes.

Jarida maarufu la uchumi duniani, Forbes lilitoa orodha ya mabilionea 21 pekee wa Afrika, tofauti na miaka mingine ambapo hutoa orodha ya matajiri 50 wa Afrika.

Kwa ujumla, mabilionea hao kutoka nchi saba za Afrika, wana utajiri wa dola za Marekani bilioni 70 ( Sh trilioni 140).

Kwa ukanda wa Afrika Mashariki, Dewji ndiye bilionea pekee katika orodha hiyo, akishika nafasi ya 16 kati ya mabilionea hao 21.

Nafasi ya kwanza katika orodha hiyo, bado inashikiliwa na Dangote kwa mwaka wa sita sasa, akiwa na utajiri wa dola bilioni 12.1 (Sh trilioni 25.4), licha ya mwaka jana kutajwa kupata hasara ya takribani dola bilioni 5 (Sh trilioni 10.05).

Nafasi ya pili inashikwa na Nicky Oppenheimer wa Afrika Kusini mwenye utajiri wa dola bilioni 7 (Sh trilioni 14.7), akifuatiwa na Mnigeria mwingine, Mike Adenuga.

Katika orodha huyo, wamo mabilionea wawili wanawake, Folorunsho Alakija wa Nigeria mwenye utajiri wa mafuta na Isabel Dos Santos, binti wa Rais wa Angola, Eduardo dos Santos.

Isabel ndiye mwanamke tajiri zaidi Afrika, akiwa na utajiri wa dola za Marekani bilioni 3.2 (Sh trilioni 6.7).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *