Mahakama ya Hakimu Mkazi upande wa utetezi leo umeieleza mahakama hiyo kuwa mmiliki wa kampuni ya kufua umeme ya IPTL, Harbinder Singh Sethi, amewekewa ‘puto’ tumboni kutokana na ugonjwa unaomkabili.

 Mtuhumiwa mwingine katika kesi hiyo ni mfanyabiashara maarufu nchini, James Rugemarila, ambapo kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 12, yakiwemo ya kutakatisha fedha na kuisababishia hasara serikali.

 Akiieleza mahakama hiyo wakili wa utetezi, Joseph Mwakandege, amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, kwamba mteja wake (Sethi) anatakiwa apelekwe kwenye matibabu Hospital ya Taifa Muhimbili lakini hadi sasa hajapelekwa, jambo linaloonyesha upande wa mashtaka umedharau amri za mahakama.

Naye wakili Joseph alisema Seth alitakiwa kwenda Muhimbili kutokana na upasuaji mkubwa aliofanyiwa na kuwekewa puto hilo tumboni la sivyo hali hiyo inaweza kusababisha akapoteza maisha kwani hospitali hiyo ndiyo yenye vifaa na watalaamu wa kutosha zaidi.

 Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali, Vitalis Peter, amedai kwamba Magereza hawapangiwi wampeleke wapi mshtakiwa ambaye ni mgonjwa bali wana utaratibu wao na hospitali maalum zenye wataalam.

 Hakimu Shahidi alisisitiza kwamba alishatoa amri mara mbili kwamba Seth akatibiwe Muhimbili. Kesi iliahirishwa hadi Septemba 14, mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *