Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili, Kampasi ya Mloganzila imezindua rasmi kitengo cha huduma ya uchujaji damu (dialysis) kwa wagonjwa wa figo.
Kitengo hicho kimezinduliwa jana Mei 8 na Makatibu Wakuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya na wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Dk. Ulisubisya alisema kitengo hicho kimewekwa jumla ya mashine 12 na kwamba kitakuwa na uwezo wa kuhudumia zaidi ya wagonjwa 10,000 kwa mwaka wakiwamo wasio na maambukizi na wenye maambukizi.
“Kitengo hiki kinachoongozwa na madaktari bingwa wazoefu na wauguzi wenye ari, kitakuwa kituo-darasa cha tiba makini kwa wagonjwa wote, vile vile kituo hiki kitatoa mafunzo endelevu kwa madaktari wajao na kitakuwa chachu ya tafiti zenye kutoa miongozo ya matibabu na kuboresha sera za matibabu ya wagonjwa ya figo nchini,” alisema.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo amesema kwa kipindi cha miezi sita hadi sasa tangu kuzinduliwa kwa MAMC tayari jumla ya wanafunzi 350 wamepokea mafunzo mbalimbali ya udaktari na udaktari bingwa.