Mkuu wa polisi katika jimbo la Catalonia nchini Uhispania, Josep Lluis Trapero, amefikishwa mahakama mjini Madrid kama mshukiwa katika uchunguzi kuhusiana na madai ya kuchochea uasi dhidi ya taifa.
Vikosi vyake vimekuwa vikishutumiwa kushindwa kulinda polisi wa taifa dhidi ya waandamanaji kabla ya kura ya maoni yenye utata juu ya uhuru kufanyika.
Afisa mwingine wa polisi wa Catalonia na wanaharakati wawili wa uhuru watahojiwa kama washukiwa.
Mzozo wa kisiasa juu ya azma ya Catalonia ya kutaka kuwa huru umewaacha maafisa wa polisi katika jimbo hilo katika hali ngumu.
Maafisa wamejipata njia panda katika kuamua juu ya utekelezaji wa wajibu wao wa kikazi wa kulinda sheria na huruma kwa wanaotaka kujitenga kwa jimbo Catalonia na Uhispania.
Wengi walichagua kutotekeleza maagizo ya kusitisha kura ya maoni ya uhuru siku ya Jumapili na kuliachia jukumu la kukabiliana na waandamanaji jeshi la polisi la serikali kuu ya Uhispania.
Kesi hizi zina uhusiano na tukio jingine la awali ambapo maafisa wa polisi walikwama miongoni mwa waandamanaji waliokuwa na hasira wakati wa uvamizi wa majengo ya serikali ya Catalonia.
Kamanda wa polisi wa Catalonia, Josep Lluis Trapero, alisifiwa kwa namna alivyoshughulikia shambulio la kigaidi la Barcelona.