Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana amesema anatamani wakuu wa wilaya za mkoa wa Dodoma wasihamishiwe maeneo mengine hadi pale azma ya serikali kuhamia Dodoma itakapokamilika kutokana na kufanya kazi kama timu.
Amesema hayo jana wakati wa mkutano wa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizungumza na makundi mbalimbali ya wananchi wa mkoani Dodoma. Rugimbana alisema wakuu wa wilaya wamekuwa wakifanya kazi nzuri kwa kushirikiana na wakurugenzi.
Amesema mkoa wa Dodoma isingekuwa rahisi kutekeleza maamuzi bila Rais John Magufuli kukubali kuibeba Dodoma.
“Wote ni mashahidi Rais baada ya kufanya maamuzi alianza kuujenga uwanja wa ndege na umekamilika awamu ya kwanza,” alisema na kuongeza kuwa amewaunganisha na taasisi na tayari wako Dodoma kuona namna ya kujipanga ili serikali kwa muda mfupi ihamie Dodoma.
“Aliitisha kikao na kukaa na taasisi za Dodoma kuona namna tunavyojipanga na usingependa kuona Dodoma haijikiti katika suala zima la mazingira,” alisema. Alisema hilo limedhihirisha ni namna gani wanaweza kupokea mji wa Dodoma hasa katika mazingira.
Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana), Antony Mavunde amesema wananchi wa mkoa wa Dodoma wako tayari kuipokea serikali kuhamia Dodoma, kwani italeta mapinduzi makubwa katika biashara na hali ya uchumi.