Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imekishauri Chama cha Wananchi (CUF) kumaliza mgogoro unaoendelea ndani ya Chama hicho kwani unaweza kusababisha kupoteza nafasi za Udiwani katika Uchaguzi Mdogo unaotarajiwa nmuda wowote kuanzia sasa.

Tahadhari hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo, Kailima Ramadhani katika mahojiano maalum Ofisini kwake kuhusu tuhuma mbalimbali zilizoelekezwa Tume hiyo ikiwemo suala la Uteuzi wa Wabunge wa Viti Maalum kupitia CUF.

Kailima amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatambua taarifa za Vyama vya Siasa iliyowasilishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa na kwa Chama cha CUF viongozi wanaotambuliwa na Tume hadi hivi sasa ni Mwenyekiti Prof. Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu ni Maalim Seif Sharif Hamad.

“Tume inatambua kuwa Mwenyekiti wa CU ni Prof. Ibrahim Lipumba, Inatambua Katibu Mkuu wa CUF ni Maalim Seif Sharif Hamad na Naibu Katibu Mkuu upande wa Bara ni Magdalena Sakaya’ amesema.

Pia amesema Tume haijazuiliwa na Mahakama wala na Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba isifanye mawasiliano na Viongozi hawa, na kubainisha kuwa Tume itaendelea kufanya mawasiliano na Viongozi mpaka hapo itakavyoelekezwa vinginevyo na Msajili wa Vyama au Mahakama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *