Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Juma Mhina ameamuru polisi wa wilaya hiyo kumkamata na kumweka ndani mtendaji wa kata ya Gelai Lumbwa, Paulo Lucas, kwa kutuhumiwa kutumia vibaya fedha zilizochangwa na wananchi wa maeneo hayo kwa ajili ya kuinua sekta ya elimu.

Baada ya Lucas kuwachenga polisi mara kwa mara, hatimaye jana agizo hilo lilitekelezwa katika maeneo ya kijiji cha Ilchang Sapukin, kata ya Gelai Lumbwa, kwenye mkutano wa hadhara wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Kabla ya Lucas kukamatwa, mwananchi Anni Mollel alimshukuru Gambo kufika katika eneo lao kujionea hali halisi ya ujenzi wa shule ya sekondari ambayo wananchi walichanga fedha zao zaidi ya Sh milioni 96 lakini hazikutumika kama ilivyokusudiwa, badala yake viongozi wa serikali na wenyeviti wa vijiji walizitumia kujinufaisha.

Baada ya Mollel kuzungumza, Gambo alimuuliza Mkurugenzi Mhina ni kwa nini hawajachukua hatua za kisheria kuwakamata watuhumiwa, ndipo Mhina aliposema mbele ya hadhara hiyo kuwa agizo lilishindikana awali baada ya Lucas kumkwepa mkurugenzi huyo mara kwa mara.

Amekamatwa jana katika mkutano huo. Mkaguzi wa ndani wa halmashauri hiyo, Mwajuma Mndaira katika taarifa yake aliyoitoa mkutanoni hapo alisema alifanya mahojiano na wenyeviti wa vijiji kujua ni kwa nini walikusanya fedha kwa wananchi pasipo kutumia risiti za stakabadhi.

Amesema pia hivi sasa bado wanaendelea na uchunguzi wa nyaraka na malalamiko ili kubaini Lucas alihusika pamoja na akina nani na kwa nini abadilishe baadhi ya matumizi kwani baadhi ya kampuni za uwindaji wa kitalii ikiwemo Wingert Windrose Safaris (WWS) na kampuni ya Kilombero Northern Safaris zilitoa mifuko ya saruji 400 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari.

Amesema wakati walipokuwa katika eneo hilo panapojengwa shule ya sekondari walibaini kuwa licha ya mifuko hiyo ya saruji kutolewa, 44 tu ndio iliyotumika huku mifuko 144 ikiwa imeuzwa na mifuko mengine 216 walidai walitumia kwenye ujenzi wa maabara na madarasa yaliyokuwa chakavu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *