Msanii wa muziki wa bongo fleva kutoka kundi la ‘Weusi’ George Sixtus Mdemu maarufu G Nako alifanikiwa kuzindua Mintape yake mpya iitwayo ‘Kiti Moto’ yenye jumla ya nyimbo tisa.
Hafla ya uzinduzi wa Mintape hiyo ilifanyika mkoani Dodoma, ikuhudhuriwa na watu mbali mbali mashuhuri huku mgeni rasmi akiwa ni Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo Mh. Innocent Bashungwa ambaye aliukata utepe wa Mintape hiyo kuingia sokoni rasmi.
Moja ya maswali ya watu wengi kwa msanii G Nako punde baada ya kulitangaza rasmi jina la Mintape hiyo kuwa ni ‘Kiti Moto’, ilikuwa ni kwanini amechagua jina hilo ambalo pengine kila mmoja anaweza kutengeneza picha yake ya tofauti alisikiapo?.
Sasa G Nako ameamua kuiweka wazi sababu ya yeye kuchagua jina hilo mbele ya Waziri Bashungwa wakati wa uzinduzi huo kwa kudai kwamba ufunguo wa kuzipeleka nyimbo kwenye ushimdani mkubwa ndani ya kiwanda cha muziki wa Afrika na Dunia ni lazima ziwe na mirindio ya kuchezeka.
“Nimeiita Minitape Yangu ‘Kiti Moto’ Kwa sababu Naamini Kabisa Bado Tunahitaji Nyimbo za Kuchezeka, zaidi ni nyimbo ambazo zinaweza kushindana na mataifa mengine kwenye Industry Kwa ujumla” alisema G Nako wakati akijibu kwa kutolea ufafanuzi sababu za kuchagua jina Kiti Moto.