Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence amesema kuwa Marekani haitaivumilia vitendo vya Korea Kaskazini.
Pence alisema hayo alipozuru eneo ambalo haliruhusiwi kuwa na wanajeshi katika mpaka wa Korea Kaskazini na Korea Kusini.
Ziara yake imetokea kipindi ambacho hali ya wasiwasi imeendelea kutanda katika rasi ya Korea, huku Marekani na Korea Kaskazini zikijibizana vikali.
Pence aliwasili mjini Seoul Jumapili saa chache baada ya Korea Kaskazini kutekeleza jaribio la kurusha kombora, ambalo halikufanikiwa.
Marekani na Korea Kusini zimeanzisha mazoezi ya pamoja ya majeshi yake ya wanahewa, kuhakikisha kwamba wanajeshi wake wako tayari kwa tishio lolote kutoka kwa Korea Kaskazini, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Korea Kusini..
Pence amesema kuwa Marekani inataka kuhakikisha kuna usalama katika rasi hiyo ya Korea “kupitia amani, kupitia mashauriano,”.
Aliyasema hayo muda mfupi baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson kusema Marekani inaweza kuishambulia Korea Kaskazini (kuzuia mashambulio ya Korea Kaskazini) alipozuru eneo hilo lisiloruhusiwa kuwa na wanajeshi mwezi uliopita.