Mgombea ubunge wa jimbo la Kinondoni kupitia tiketi ya CHADEMA, Salum Mwalimu amekitahadharisha Chama cha Mapinduzi kuwa uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo mawili CHADEMA haitakuwa na muda wa kulialia badala yake watapambana kwa kila aina kupata haki stahiki.
Mwalimu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar amedai kuwa katika uchaguzi huo yupo mbele katika kutetea maslahi ya wananchi wa Kinondoni hivyo atapigania haki kwa kila aina.
“Kama ni nidhamu ya siasa waliyoikataa hapa watairudisha, na wasipokubali kuirudisha Kinondoni maana yake ustaarabu katika siasa tunaamini utakuwa umeshamalizika, hatutakuwa wakulia safari hii kama ikibidi tutasababisha wale waliokuwa wanatufanya sisi tunalialia hao ndio walie. Nimedhamiria kuitafuta haki ya watu wa Kinondoni, nimejitoa katika kusimamia haki ya watu Kinondoni sitoyumba.“amesema Mwalimu mbele ya Waandishi wa Habari wikiendi iliyopita mapema baada ya kurudisha fomu yake ya kugombea ubunge.
Kwa upande mwingine Mwalimu aliwasilisha pingamizi kwa mgombea ubunge kwenye jimbo hilo kwa tiketi ya CCM, Ndg Maulid Mtulia kwa kutoa hoja tano ikiwemo ya kutorudisha mrejesho wa gharama za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, wakati akigombea ubunge akiwa CUF.
Wakati hayo yakiendelea jijini Dar es salaam, kule mkoani Kilimanjaro katika jimbo la Siha kampeni zimeanza ambapo CCM kupitia kwa mgombea wao Dkt. Gabriel Mollel wanachuana vikali na Elvis Mosi wa CHADEMA.
Uchaguzi wa majimbo mawili ya Kinondoni na Siha umekuja baada ya waliokuwa wabunge wa majimbo hayo kuhamia CCM na uchaguzi huo mdogo unatarajiwa kufanyika mnamo tarehe 17 Februari mwaka huu.