Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire amemuomba Rais Dkt. John Pombe Magufuli kukutana naye ili amueleze kinachosababisha malumbano na viongozi wenzake jijini hapo.

Bwire amemueleza hayo Rais Magufuli leo eneo la Igogo alipopata nafasi ya kuwasalimia wananchi wa Mwanza na kutoa salam za pongezi kwa Rais ambaye yupo ziarani mkoani humo kufungua viwanda na miundombinu mbalimbali ya kiuchumi.

Meya James Bwire alikamatwa jana na Jehi la Polisi huku ikidaiwa kuwa amri ya kukamatwa kwake ni agizo la mkuu wa mkoa huo, John Mongella ambapo hata hivyo baadaye aliachiwa huru kwa dhamana.

Hata hivyo, Mongella alikana kuamuru kukamatwa kwa kiongozi huyo anayeshikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Jiji la Mwanza

Bwire alikamatwa katika Uwanja wa Ndege Mwanza wakati wa mapokezi ya Rais John Magufuli ambaye ziko ziarani mkoani humo kwa madai ya kutaka kufanya kitu kibaya kwenye msafara wa Rais.

Tangu Aprili, Bwire na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba wamekuwa katika mgogoro kila upande ukiutuhumu mwingine kuhujumu shughuli za maendeleo.

Aidha akihutubia katika Viwanja vya Nyakatio jana, Rais Magufuli aliwataka Meya, James Bwire na viongozi wenguine wa mkoa huo (ambao hakuwataja) wamalize malumbano yao ili wawatumikie wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *