Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita leo amesitisha  mkataba na Kampuni ya Mwamkinga Auction Mart and Brokers iliyokuwa ikifanya kazi ya kudhibiti uegeshaji wa magari katika maeneo yasiyo rasmi katika Halmashauri ya Temeke na Kigamboni.

Mwita amesema amefikia uamuzi huo kutokana na kampuni hiyo kufanya kazi kwa kutozingatia matakwa ya mkataba na hivyo kuanzisha migogoro isiyo ya lazima baina ya halmashauri ya jiji na wananchi.

 Amefafanua kuwa jiji liliingia mkabata na kampuni hiyo Aprili mwaka huu kwa lengo la kufanya kazi hiyo ambapo mkataba huo ulielekeza kufanya kazi kwa weledi mkubwa, kuzingatia sheria, miongozo, maelekezo, kanuni na taratibu zilizopangiwa bila kusababisha bughudha, uonevu, kero na usumbufu kwa wananchi, jambo ambalo halikufanyika.

Amesema kampuni hiyo inapaswa kuondoka mara moja kwenye maeneo iliyopangiwa kufanya kazi hiyo na kuhakikisha kwamba kuanzia tarehe ambayo mkataba huo umesitishwa iwe imekabidhi mashine zote za kukusanyia mapato kwa halmashauri zikiwa katika hali salama.

Aidha Mwita amesisitiza kuwa hatasita kuzichukulia hatua kampuni nyingine ambazo zimepewa tenda hiyo na kuzionya kuwa iwapo wana tabia hiyo waache mara moja kwani kazi waliyopewa si ya kunyanyasa wananchi bali ni kufanya kazi kwa kufuata sheria.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *