Meneja wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, Salaam Sharaf amefunguka sababu ya mwanamuziki wake huyo kuita wimbo wake mpya kwa jina la “Hallelujah’.
Salaam amesema kuwa jina la wimbo huo limetumika kama kionjo cha kusifu uumbaji wa Mungu na si kama wengi wanavyotafsiri.
Salaam hakuishia hapo alitolea mifano ya baadhi ya wasanii hapa nchini ambao wamewahi kuweka neno Mashaalah katika nyimbo zao, huku wengine wakitumia neno Halelluya maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi akiwemo mwanamuziki Nameless katika wimbo wake “Nasinzia”.
Salaama amesema kuwa “Wakati anatunga mashairi yake lengo lilikuwa kusifia uumbaji, mbona wapo wasanii wengi hapa nchini wametumia neno Mashaallah, Hallelujah maana yake ni kumtukuza na kumsifu Mungu lina tofauti gani na Mashaalah?”.
Pia amesema watu wanaozungumzia suala hilo wanatafuta namna ya kuonekana wanaongea na iwapo wanaona kuna mahali mambo hayajakaa sawa ni vema wakaenda kwenye vyombo vya sheria, “Nafikiri hawana jipya wameshindwa watasema nini kuhusu wimbo huu, hawana sababu ya msingi.”