Kamati ya Bunge, Viwanda, Biashara na Mazingira imesema meli mbili za mafuta ghafi zimekwama katika bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya wiki mbili sasa kutokana na utata wa kodi inayotakiwa kulipwa.
Kufuatia hali hiyo, Serikali imeagizwa kulitafutia ufumbuzi suala hilo kwa kuwa linaweza kusababisha uhaba wa bidhaa zingine zinazotokana na mafuta hayo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Suleiman Sadiq Murad, katika semina ya kuwajengea uwezo wabunge kuhusu utendaji kazi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na Tume ya Ushindani (FCC).
Murad alisema kuna meli mbili zipo bandarini zimeleta mafuta hayo na kwamba Mkemia Mkuu, TBS wametoa cheti) kwamba ni ‘mafuta ghafi, lakini Mamlaka ya Mapato (TRA) imekataa, ikisema sio mafuta ghafi.
Alitoa tahadhari kwa serikali kuwa mafuta ya kula yameanza kupanda bei kwa sababu mafuta ghafi yaliyoko nchini yanatumika na viwanda havitakuwa na malighafi tena ya mafuta ghafi.
Mwenyekiti huyo alisema kuna tatizo na lipo bandarini na kumuomba Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, aliyekuwapo katika kikao hicho kwenda kulitafutia ufumbuzi.
Akizungumzia suala hilo, Manyanya alisema suala la uagizaji mafuta lina uhusiano mkubwa sana na masuala ya kiuchumi katika nchi.
Awali, akitoa mada Kaimu Mkurugenzi wa TBS, Tumaini Mtitu, alisema shirika hilo linakabiliwa na upungufu wa vifaa vya kupimia bidhaa kwa sababu ya ufinyu wa nafasi ya maabara 24 na gharama ya kuvinunua.